Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Maofisa Mawasiliano wa Serikali (TAGCO) unatarajiwa kufanyika mkoani Morogoro kuanzia tarehe 08-12 APRILI 2025.
Kwa Mujibu wa Mwenyekiti wa TAGCO Bw. Karimu Meshack, katika Mkutano Mkuu wa mwaka huu 2025 zaidi ya wataalam 500 wa Mawasiliano wa Serikali wanatarajiwa kushiriki ambapo mada mbalimbali zitakazojadiliwa katika mkutano huo zitalenga kuwaongezea maarifa watalaam wa Mawasiliano na Uhusiano wa Serikali ili kuongeza kasi katika kuisemea Serikali kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Tunatarajia kuwa na washiriki zaidi ya 500, viongozi wa TAGCO tumeandaa wataalam wabobezi ambao tutashirikiana nao kujadili mada mbalimbali zinazoendana na wakati wa sasa ili kupanua wigo wa uelewa kwa Wananchama wetu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku” aliongeza Bw. Meshack.
Meshack ameongeza kuwa katika mkutano huo TAGCO inatarajia kuwasilisha marekebisho ya katiba yake ili yajadiliwe na kupitisha kuendana na mahitaji ya Chama kwa sasa na kutumika kama nyenzo muhimu ya utendaji wa Chama cha Maofisa Mawasiliano wa Serikali.
Kwa wataalam wote wa Mawasiliano ya Serikali ambao wanatarajia kuhudhuria Mkutano huo wa Mwaka watapaswa kujisajili kwa njia ya mtandao kupitia kiunganishi https://agm.tagco.go.tz

